Dalili za Marejeo -1

DALILI ZA KURUDI KWA YESU SEHEMU YA KWANZA.

  • Wasomaji makini wa maandiko wanaona bayana utimilifu alama za nyakati.
  • Ving’ora vinalia na kengele za hatari zinasikika zikiutangazia ulimwengu huu kuwa mwisho wake umefika.
  • Pamoja na ushahidi mkubwa unaoonyesha kuwa tuko ukingoni mwa dunia hii, wengi wetu tumelala usingizi mzito, hatujafungua masikio na macho yetu ili tusikie na kuona utimilifu wa dalili za nyakati za mwisho.

Leo tutatafakari juu ya mada hii.

Dalili za Siku za Mwisho

Wanafunzi walimwuliza Yesu wakisema; ” .. Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?”(Mathayo 24:3.) Yesu akaanza kuzitaja:

Manabii na Makristo wa Uongo WataongezekaYesu akasema; “.. wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.” Sehemu nyingine imeandikwa; “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele” (Mathayo 24:5,11, 24.)

MANABII WA UONGO

Dalili ya kwanza kabisa aliyoitaja Yesu na aliyorudia sana kama alivyonukuriwa na Mathayo ni kuongezeka kwa manabii na wanaofundisha ukristo wa uongo.

Taarifa za kiutafiti zinaonyesha kuwa hivi sasa kuna aina za dini (yaani ukristo, uislam, ubudha, uhindu, n.k) takribani 4,200.
Lakini pia, hivi karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya kuongezeka kwa makanisa (madhehebu) ya kikristo: mpaka mwaka 2001 kulikuwa na aina ya makanisa 34,000,  miaka 10 tu baadaye, yaani 2010 yalikuwa 41,000 na kwa kasi hiyo ya kuongezeka inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2025 kutakuwa na madhehebu ya kikristo yapatayo 55,000.
(chanzo: World Christian Encyclopedia na Christian Encyclopedia unaweza kuzipata encyclopedia hizi kwenye mtandao wa internet).

Ingawa makanisa haya yanatofautina sana katika imani za msingi, kila moja linajiita ndilo la kweli na kwamba linamhubiri Kristo. Hii imewachanganya wengi sana, mamilioni kwa mamilioni sawa sawa kabisa na unabii huu.
Wengi, wengi sana wamekuwa mateka kwa sababu ya kukosa maarifa juu ya neno la Mungu.

Yesu akiwa kama Mungu aliona kwa mbali juu ya udanganyifu huu akasema; “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. .. Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” (Mathayo 7:15-23.)
Yesu alitoa mwongozo wa kuwawezesha watu kujua ni yupi wa kweli na yupi ni wa uongo akisema – wakristo wakweli watafundisha mapenzi ya Mungu yaani maagizo yote na sheria zote za Mungu na ushuhuda wa Yesu
ufunuo 14 :12 Hapa ndipo penye subira ya Watakatifu, wazishikao amri za Mungu na imani ya Yesu.


 

Vita na Machafuko Kuongezeka

Yesu aliendelea kusema; “Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme;” Mathayo 24:6-8.

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vita na kila aina ya mapigano na machafuko. Taarifa zinaonyesha kuwa karne ya 20 ilikuwa ni karne ya umwagaji mkuu wa damu kuliko zote.
Kulikuwa na vita Kuu ya 1, iliyogharimu maisha ya watu milioni 20; vita kuu ya 2 milioni 50 na nyingine nyingi.
Hali kadhalika karne ya 21 kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara, sehemu nyingi za dunia. Tumeshuhudia vita Darfur, Libya, Yemen, Afghanistan, Ukraine, Rwanda, Syria, Irak, Congo, Sudan Kusini, n.k.

Mtiririko wa mapigano ya nchi na nchi, na yale ya makabila ama makundi kama vile Boko Haram, Al-Shabab, Al-Quida n.k. nayo pia yameongezeka sana.

Takwimu zinaonyesha kuwa, matukio ya vita zote kwa mwaka (yaani vita kati ya nchi na nchi, na vile vya ndani ya nchi [makabila, makundi ya kijamii]) imeongezeka kwa zaidi ya 400% kutoka 40 kwa mwaka (1946) hadi zaidi ya 160 kwa mwaka (1990). (Chanzo: Centre for Systemic Peace, Viena Austria http://www.historytoday.com). Hali ni tete, watu wamekuwa waovu wasiotaka amani.

Tutaendelea na uchambuzi wetu wa utimilifu wa dalili hizi alizozitaja Yesu. Lakini leo itoshe kujua kuwa; “myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia” Yesu anasema “jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”(Mathayo 24:33,34,44.)

Mungu akubariki sana unapotafakari somo hili la leo.

Itaendelea, dalili za kurudi kwa Yesu sehemu ya pili.