Majaribu -2

Nini cha kufanya uwapo katika jaribu?

Kuna makosa makubwa mawili ambayo Wakristo wengi tunayafanya tuwapo katika majaribu. Na makosa haya ndiyo yanayogharimu uhusiano wetu na kutufarakanisha na Mungu. Makosa hayo ndiyo yanayofanya tunaangushwa na majaribu.

Kosa la kwanza; tunatumia akili zetu kutafuta ufumbuzi wa jinsi gani tutavuka jaribu tunalopitia kwa ushindi na kumuacha Mungu kando ambayo ndiye msaada wetu. Hapa ni lazima uelewe, Mungu pekee ndiye anayetushindia majaribu, kwa akili zetu na nguvu zetu na maarifa yetu hatuwezi kamwe kujinasua katika majaribu. Uwapo katika jaribu ni lazima umkabidhi Mungu njia zako na jaribu lako, Yeye ndiye ushindi wako kwa Jina la Yesu Kristo (2 Petro 2:9, Zaburi 37:5)

Kosa la pili; kuwaangalia wanadamu wanafanya nini na wanasema nini tunapopita katika jaribu hasa wapendwa au wakristo wenzetu. Kitu tunachojisahau hapa ni kwamba tunategemea wingi wa marafiki tunaokuwa nao wakati wa furaha ndio hao hao tutakao kuwa nao wakati wa majaribu, sivyo! Uwapo katika shida au jaribu kama kuna mkristo mwenzako atabaki na wewe hiyo ni neema tu ya Mungu, lakini wengi kama siyo wote watakuacha peke yako.

Unajua kwa nini watakuacha peke yako? Jaribu siyo lao ni lako, anayepaswa kushinda siyo weo ni wewe. Kwa hiyo ni lazima upite peke yako ili ushinde peke yako na tuzo ya ushindi utapata peke yako. Hupaswi kuwaangalia wapendwa na hupaswi kulalamika iwapo watakuacha upite katika jaribu peke yako.
Hebu tuangalie mfano; kuna wakati Yesu Kristo alizuiliwa na Wasamaria kuingia katika kijiji chao, Yakobo na Yohana walichukizwa na jambo hilo na wakataka kuagiza moto kutoka mbinguni ili kuwaangamiza Wasamaria wale lakini Yesu Kristo aliwazuia (Luka Mtakatifu 9:51-56)

Ilipofika wakati Yesu Kristo anakikabiri kikombe cha mateso, baada ya kuila pasaka aliwachukua wanafunzi wake hadi bustani ya Gethsemane na akawachukua Petro, Yakobo na Yohana kwa ukaribu zaidi. Akawaambia Roho yangu ina huzuni kiasi cha kufa, kaeni hapa mkeshe pamoja nami (muombe pamoja nami), lakini wanafunzi hawa walipofika sehemu hii walilala wakamuacha Yesu Kristo apambane mwenyewe. Kwa sababu hawakua na sehemu ya kukinywea kikombe cha mateso cha Yesu Kristo (Mathayo Mtakatifu 26:36-40)

Kwa hiyo ninataka utambue kuwa uwapo katika jaribu hupaswi kutumia akili, ufahamu, elimu na nguvu zako kujinasua kutoka katika jaribu. Mruhusu Mungu akuvushe mwenyewe kwa utukufu wake kwa jina la Yesu Kristo. Pia ni lazima wapendwa au wakristo wenzako wakuache ili uvuke wewe mwenyewe kwa sababu unayejaribiwa ni wewe na siyo wao.

Namna ya kupita katika jaribu ili upate ushindi wa heshima
Hapa ndipo penye kiini cha somo hili, namna unavyopita katika jaribu ndivyo kunaamua namna na aina ya ushindi utakao upata. Ukipita kwa akili zako utapata matokeo yanayolingana na akili yako, na hata ukishinda hutapata ushindi wa heshima wenye utukufu wa Mungu. Kwa mfano wapo mabinti wawili wanatafuta kazi, mmoja akatumia mwili wake (rushwa ya ngono) na mwingine akamtumaini na kumtegemea Mungu, wote wanaweza kupata kazi, lakini furaha ya kupata kazi na utukufu wa kazi utatofautiana na hata muda wa kudumu katika kazi utatofautiana pia.

Unapopita katika jaribu, ni lazima uzingatie mambo yafuatayo ili Mungu akupiganie na upate ushindi wenye sifa na utukufu kwa Mungu, ushindi wenye taji safi kwa imani na ushuhuda wako.

UTII KWA SAUTI YA NUNGU

Unapokuwa na jaribu shetani huongea mara nyingi kwa sauti nyingi, lakini Mungu huongea mara chache sana kwa sauti moja tu. Ni lazima ukubali kuisikiliza, kuitambua na kuitii sauti ya Mungu, huo ndio ushindi wako.

Yoshua 6:3-4. “Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao.”

Kabla ya kufika katika mji wa Yeriko, Israeli walipigana vita vingi na kama ni ujuzi wa vita basi walikuwa nao. Wangeweza kuingia Yeriko pasipo kumshirikisha Mungu kwa sababu vita nyingi walizopigana walishinda, walikuwa na kila sababu ya kumshirikisha Mungu na kushinda pia.