MAJARIBU

🌹MAJARIBU🌹
MAANA NA MAKUSUDI YA KUJARIBIWA

Familia zetu Mara nyingi hukumbwa na majaribu. Kwann?
Jaribu linasemekana kuwa ni mtaji wa kuinua imani ya mtu anayejaribiwa, lakini binafsi ninapenda kuirekebisha sentensi hii. Jaribu ni mtaji wa kuinua imani ya anayeshinda jaribu; kama umejaribiwa na jaribu likakuangusha, siyo sahihi kusema jaribu hilo lililokuangusha lilikuwa mtaji wa kuinua imani yako. Imani ipi? Kama umeshindwa kuitetea imani yako na kuangushwa, jaribu halikuwa mtaji kwako.

Jaribu huja na makusudi mawili; moja, ni kumuimarisha kiroho na kuinua imani ya anayejaribiwa na kushinda jaribu. Pili, ni kumuangusha mtakatifu na kuharibu uhusiano wake na Mungu. Na mara nyingine jaribu au teso huwa ni kiboko cha Mungu cha kulirudi kanisa lake. Ninaposema kanisa ninamaanisha Mkristo.

Kuinua imani ya Mkristo. Nikupe mfano kwanza, kuna hekima ya Kimungu na hekima ya kibinadamu. Hekima ya Kimungu hupewa mtu yoyote pasipo kujari umri, na hii huletwa na Yesu Kristo mwenyewe. Na hekima ya kibinadamu huja kutokana na uzoefu wa muda mrefu alionao mtu katika jambo fulani, na hekima hii wanayo wazee. Na imani ndivyo ilivyo, ili ikue ni lazima ipitishwe katika kujaribiwa, ipitishwe katika vitu ambavyo sayansi na akili ya kibinadamu haviwezekani. Ukiisha pita hapo kwa msaada wa Mungu kwa jina la Yesu Kristo ndipo imani yako inapokuwa. Ndipo unapozidisha imani na uhusiano wako na Mungu kupitia Yesu Kristo (Yohana 11:3-4, 14-15 na 1 Petro 1:6-7)

Kumuangusha mtakatifu. Hili ni jaribu linalosababishwa na shetani moja kwa moja, na makusudi yake huwa ni kumuangusha mtakatifu ili kuharibu na kufuta kabisa uhusiano wake na Mungu. Kwa mfano, Ayubu hakujaribiwa ili kuinua imani yake au kurudiwa na Mungu, alijaribiwa ili amkufuru Mungu, kwa Kiswahili chepesi ni ili avunje uhusiano wake na Mungu. Kwa hiyo kuna wakati shetani huwajaribu Wakristo ili awafarakanishe na Mungu (Yohana 2:10, Ayubu 2:4-5)

Kurudiwa na Mungu. Hapa naomba nieleweke, hili kwa upande mmoja siyo jaribu na kwa upande mwingine ni jaribu. Nina maana gani; kwa upande wa Mungu ni kiboko cha kulirudi kanisa lake kama ilivyo kwa mzazi anapomuadhibu mtoto aliyekosea. Kwa upande wa Mkristo, analiona kama jaribu. Na hili hutupata ikiwa tumekengeuka na kuiacha njia ya haki, tumemkosea Mungu. Na tukitubu na kuirudia njia ya haki, utaona mateso yote yanaondoka pia (Mithali 3:11-12, Ayubu 5:17)