ZABURI 117

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO


MUHTASARI WA ZABURI 117     

  • Neno Kuu: Msifuni Bwana; f. 8.
  • Tabia ya Mungu: Upendo, Rehema, Uaminifu
  • Mistari Ya Msisitizo: Zaburi 117:1-2
  • Wahusika: Watu wote

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

 

ZABURI 117

1 Haleluya. Enyi mataifa yote, msifuni Bwana, Enyi watu wote, mhimidini.

2 Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu, Na uaminifu wa Bwana ni wa milele.

 


 

Hii ndiyo sura fupi kuliko sura zote katika kitabu cha Zaburi, lakini ni sura ya kuzingatiwa katika maudhui yake. Utabaini ya kwamba hakuna kabila au taifa lolote lililoachwa katika mwaliko huu wa kumsifu Bwana. Katika Warumi 15:11 mtume Paulo akizungumzia sura hii anadhihirisha kwamba katika Kristo, huruma ya Mungu imeendelea hadi kwa Wayunani na Wayahudi.

Katika aya hizi mbili peke yake tunaweza kuona sifa za kutosha kuhusu Mungu kumpenda na kumsifu Yeye. Sifa ya Mungu iliyotolewa katika sura hii ni ya milele kama Mungu mwenyewe, na kuandikwa kutukumbusha kwamba katikati ya changamoto zinazotuzunguka, tunaweza kupumzika salama katika upendo wa Mungu.

Bwana anasubiria tuzitangaze fadhili Zake na kuwaambia walimwengu uwezo Wake. Anatukuzwa na kuhimidiwa katika  sifa na shukrani zetu. Mungu anatamani kwamba maisha yote ya watu Wake yawe maisha ya sifa na kumtukuza Yeye. Maisha haya yatafukuza roho ya manunung’uniko na malalamiko. Ushuhuda wa shukrani utawashawishi wengine na itakuwa njia mojawapo ya kuongoa roho nyingi  kwa Kristo.

Jan Harry Cabungcal

  • Neuroscientist
  • Europe for Jesus
  • Uswisi

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu mpendwa, tunashukuru kwa tafakari ya Neno Lako katika sura hii. Twaomba Roho Wako aendelee kutufundisha sura hii tena na tena. Tukumbushe kuyasoma maandiko, na kuendelea kuyasikia “maneno ya Unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”.Tusaidie kuwa “watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali tukijidanganya nafsi zetu”. Ebu mmoja aguswe na kubadilishwa na Neno hili zuri la Kristo Yesu. Asante Bwana, na twaja katika Jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mkombozi wetu, Amina!